CHAMA cha ACT-Wazalendo kinachoongozwa na Zitto Kabwe, kimempongeza Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, kwa kushinda kiti cha urais wa Chama cha Wanasheria (TLS) katika uchaguzi uliofanyika juzi jijini Arusha.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Naibu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Msafiri Mtemelwa, alisema Lissu anastahili pongezi kwa kufanikiwa kushinda nafasi hiyo kutokana na changamoto zilizomkumba katika kuisaka.
Alisema kuwa licha ya kupitia misukosuko mingi iliyokuwa inaonyesha njia ya kumkwamisha kufikia malengo yake, Lissu hakukata tamaa na alionyesha ujasiri.
Mtemelwa alisema kupata nafasi hiyo kwa kiongozi kutoka upinzani ni dalili njema na kipimo kwa wapinzani na kwamba anapaswa kuitendea haki nafasi hiyo kwa ustawi wa vyama hivyo vya upinzani.
“Mimi niseme tu kwamba, Lissu anastahili pongezi," Mtemelwa alisema. "Tunahitaji watu kama hawa, watu majasiri. Pamoja na kwamba alipata misukosuko mingi, alipambana na akapenya.
"Sisi tuliopo upinzani, tunajua palivyopagumu, tunapambana sana na kukamatwa kamatwa. Pasipo kupambana, huwezi kupenya.
Kwa hiyo, (Lissu) anastahili pongezi, amepambana na hii ni ishara na kipimo kizuri kwa wapinzani, anatakiwa kufanya mazuri ili awaonyeshe kwamba wapinzani wanaweza, italeta sifa nzuri kwa wapinzani, vivyo hivyo akifanya vibaya italeta sifa mbaya."
Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), aliibuka kidedea katika uchaguzi huo akipata kura 1,411 kati ya 1,682 zilizopigwa.
Kabla ya uchaguzi huo, Lissu alikumbana na changamoto kadhaa ikiwa ni kufunguliwa kwa kesi Dar es Salaam na Dodoma na mawakili wawili wakitaka usimamishwe kwa madai ya kuwapo kwa kasoro katika kanuni za uchaguzi huo.
Aidha, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe, pia alikaririwa akitishia kukifuta chama hicho iwapo kitakuwa na mwelekeo wa kisiasa kauli ambayo ilionekana kumlenga Lissu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)