Yanga Mzuka Umepanda,Matajiri Wamwaga Pesa kwa Wachezaji..!!!


MZUKA umekolea Yanga. Hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya matajiri wa Yanga kumwaga fedha na kuweka mambo sawa kuelekea mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zanaco ya Zambia utakaochezwa kesho kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Matajiri wa klabu hiyo wamelipa malimbikizo ya madeni yote waliyokuwa wakidai wachezaji wao akiwamo beki wa kati, Vincent Bossou, kwa lengo la kuwaongezea morali ya ushindi dhidi ya wapinzani wao.

Akizungumza jana, Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa, alisema wachezaji waliokuwa wanaidai klabu hiyo wamelipwa.

Mkwasa alisema kwa sasa hakuna mchezaji anayedai na kila mmoja amelipwa kutokana na stahiki yake na kazi iliyobaki ni kusaka ushindi dhidi ya Zanaco.

“Hakuna mchezaji yeyote anayeidai Yanga, Bossou alikuwa anatudai mshahara wa Februari mwaka huu na limbikizo la fedha zake za Agosti mwaka jana,” alisema Mkwasa.

Mkwasa alisema limbikizo la fedha hizo si mshahara nazo amelipwa ili waweze kuitumikia klabu yao kwa asilimia 100.

Kiungo huyo wa zamani wa Yanga, alisema lengo la kuwaweka sawa wachezaji ni kuhakikisha wanaondoa na kuziba mwanya wa wachezaji wao kulalamika au kuwa na mawazo yatakayowafanya wacheze huku wakiwaza mambo ya nje ya uwanja.

Alisema wamelazimika kufanya hivyo kwa lengo la kuwapa hamasa wachezaji wao kupata ushindi mkubwa katika mechi ya kwanza ili kuwarahisishia kusonga mbele kwenye michuano hiyo.

“Kama utawala tumehakikisha tumeweka mambo yote sawa kwa sababu tunatakiwa kushinda mechi hii ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele, kama unavyojua tukishindwa kupata ushindi hapa nyumbani kazi itakuwa ngumu ugenini,” alisema Mkwasa.

Katika hatua nyingine, kocha msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi, alisema wamewasoma wapinzani wao kupitia mikanda ya video (CD) kwa mechi walizocheza, lakini hawataingia uwanjani kwa kutegemea mbinu moja, wamejipanga kupambana kutafuta matokeo mazuri.

“Tuna wachezaji na kocha wametokea Zambia ambako Zanaco wanatoka, lakini soka linabadilika, unaweza kuangalia mechi leo lakini kesho ukacheza ukakuta kikosi kimebadilika, hivyo tunajiandaa kama sisi na si kutegemea mtu wala CD,” alisema Mwambusi.

Mwambusi alisema kwa kawaida Yanga ina kikosi kipana ambapo hata michezo ya nyuma wanakuwa na majeruhi lakini matokeo mazuri yanapatikana.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano wa Yanga, Paulo Malume, alisema kurejea kwa Donald Ngoma na Thaban Kamusoko, kumewafanya wachezaji kuwa na morali ya hali ya juu kuelekea mechi hiyo.

“Tumejiandaa vizuri kama ulivyoona timu iko mazoezini, waliokuwa majeruhi wamerudi, ni raha kwa kweli tuna imani kocha kesho atapanga ‘full muziki’ kama hakutatokea mabadiliko yoyote kikosini,” alisema Malume.

Alisema katika kuhakikisha wanawapa morali vijana wao matajiri wa timu hiyo, wamechanga kiasi cha fedha kuwapa endapo wataibuka na ushindi.

“Kama ilivyo kawaida yetu wachezaji wakifanya vizuri tunawapa tuzo, tumekuwa na utaratibu wa kukutana katika vikao vyetu na tuna fedha zipo tayari siwezi kuzitaja ni kiasi gani ili kuwapa wachezaji wakishinda,” alisema.

Zanaco waliwasili jana tayari kwa mechi huku nahodha wa timu hiyo, Ziyo Tembo, akimtaja kiungo wa Yanga Mzambia, Justine Zullu, kuwa wanamjua uwezo wake ndani na nje ya uwanja.

Akizungumza baada ya kuwasili katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Tembo alisema kiungo huyo wa Yanga hawezi kuwasumbua huku kocha wao, Munamba Numba, akitamba kuondoka na ushindi.