Bongo Muvi Mnazingua Mjue...!!!!


SOKO la filamu za Kibongo lipo hoi, linasuasua. Sababu za kusuasua huko zimetajwa nyingi, lakini hivi karibuni kuna kundi kubwa limeibuka na kudai kuwa eti wasanii kujiingiza katika siasa kumesababisha anguko hilo.

Hoja ya ajabu kabisa. Wanadai eti kwa sababu mastaa kadhaa wa Bongo Muvi walionyesha upande wao wa kisiasa na ama kushiriki kwenye kampeni za kambi mbalimbali za vyama vya siasa kulichangia kurudisha nyuma soko la filamu nchini.

Si kweli. Wasanii wenyewe ndiyo wanaozingua. Nitajenga hoja.



TUANZE NA WEMA SEPETU

Hivi karibuni actress mwenye mashabiki lukuki, Wema  Sepetu aliamua kujiunga na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Staa huyo ambaye ni Miss Tanzania mwaka 2006, alikuwa kada kindakindaki wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mbali ya kuwa mstari wa mbele katika kuwanadi wagombea wa CCM katika Uchaguzi Mkuu mwaka juzi, pia aligombea Ubunge wa Viti Maalum mkoani Singida – kura hazikutosha.

Akiwa CCM, katika kipindi cha kampeni, Wema alikuwa na wenzake wengine kama Yobnesh Yusuph ‘Batuli’, Steven Mengele ‘Nyerere’, Vincent Kigosi (awali alikuwa Chadema – Ukawa) na wengine wengi.



MASTAA NA SIASA

Mbali na hao, wasanii wengine walioshiriki kwenye kampeni na kujitanabaisha wazi kuwa ni wanachama wa vyama mbalimbali na hasa CCM na Ukawa ni pamoja na Jacob Stephen ‘JB’ na Wellu Sengo.

Wengine ni Single Mtambalike ‘Richie’, Deogratius Shija, Chuchu Hans, Jeniffer Kyaka ‘Odama’, Aunt Ezekiel, Mahsein Awadh ‘Dokta Cheni’, Jacqueline Wolper na wengineo.

Ukiacha mastaa hao wa filamu, wapo wanamuziki kadhaa ambao nao walishiriki kwenye kampeni hizo, miongoni mwao ni staa wa Bongo Fleva anayeendelea kupasua anga za kimataifa, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Emmanuel Elibariki ‘Ney wa Mitego’ na Kala Jeremiah.

Lakini wapo waliojitosa kugombea katika majimbo  mbalimbali kama Afande Sele (Morogoro Mjini – ACT – Wazalendo), Mohamed Mwikongi ‘Frank’ (Segerea – ACT – Wazalendo), Rashid Mwinshehe ‘Kingwendu’ (Kisarawe – CUF) na wengineo.



WALIOTUSUA KWENYE SIASA

Ipo mifano kadhaa ya wasanii wa sanaa mbalimbali duniani ambao waliingia kwenye siasa na kufanya vizuri. Kwa hapa kwetu mfano mzuri ni wabunge Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ (Mbeya Mjini) na Joseph Haule ‘Profesa Jay’ (Mikumi), wote wa Chadema.

Profesa Jay ni mara yake ya kwanza kuingia bungeni, lakini Sugu aliingia tangu bunge lililopita ambapo takwimu zinasema, alikuwa mgombea pekee aliyeshinda kwa kura nyingi zaidi kuliko mgombea yeyote!

Tuwaache hawa, twende kimataifa. Msanii maarufu wa filamu nchini Nigeria, Desmond Elliot ni mbunge na alimshinda mshindani wake wa karibu Bayo Smith kwa karibu zaidi ya nusu ya kura zote.

Lakini mwigizaji wa Hollywood Arnold Schwarzenegger, amepata kuwa Gavana wa Jimbo la California.

Je, ni kweli kwamba wasanii hao wote baada ya kuonyesha upande wao wa kisiasa, waliwagawa mashabiki, hawakubaliki na wamepoteza mvuto? Jibu ni hapana.



UKWELI NI HUU

Siasa ni maisha. Kupenda chama fulani au kuwa shabiki wa chama fulani ni haki ya kila binadamu. Jambo la msingi ni kuridhika na sera za chama husika. Sioni tatizo kwa Steve Nyerere kuwa CCM huku akiwa mchekeshaji. Hakuna dhambi kwa JB kuwa CCM wakati akifanya sinema zenye viwango.

Hakuna uhusiano wowote kati ya ubunge wa Sugu na muziki wake kama msanii. Kuwa mwanasiasa ni kuchagua kuwawakilisha wananchi. Hakuhusiani na sanaa.

Kinachopendwa na mashabiki ni namna msanii anavyofanya vizuri kwenye sanaa yake na siyo dini, itikadi ya chama wala jina lake.

Kama ingekuwa kuonyesha upande kisiasa ni kujiua kisanii bila shaka Diamond (CCM) angekuwa ameshapotea kwenye soko la muziki, lakini ndiyo kwanza anapeta na Marry You – kibao alichomshirikisha mkali wa sauti kutoka Marekani, Ne-YO.


TATIZO NI LILELILE

Kinachoitafuna Bongo Muvi ni kilekile. Ubunifu, skendo (kiki), kuvamiwa kwa sanaa na watu wasio wasanii na mengine kama hayo.

Kamwe Bongo Muvi haitarudi kwenye heshima yake ikiwa hadithi zitaendelea kuwa mbovu, wasanii hawatajitambua na kuwa na ushindani. Msijifiche kwenye hoja ya siasa.

Natamani enzi za Shakira, Sikitiko Langu, Born Again,  Oprah, Agano la Urithi, Misukosuko, Girlfriend, Simu ya Kifo, Odama na  Fungu la Kukosa.

Nimezikumbuka sana enzi za White Maria, Fake Pastors, Village Pastor, Hostel, Behind the Scene, Swahiba, Gentlemen na Red Valentine.

Rudini hapo. Acheni maneno, fanyeni kazi. Wapo wachache wanaojitahidi, lakini wengi wanaoharibu wanalididimiza soko la filamu nchini. Ni tamaa yangu siku moja muinuke tena.