Mrema Aunga Mkono kauli ya Rais Magufuli .....



Mwenyekiti wa TLP taifa Dkt. Augustine Lyatonga Mrema amesema kwamba kitendo cha Rais Dkt. John Magufuli kusema kwamba siasa ziachwe hadi miaka mitano iishe kunatokana na tabia ya upinzani kugomea kila kitu bila kuweka maslahi ya taifa mbele.

Dkt. Mrema ameyasema hayo leo alipokuwa akizungumzia  kuhusu kauli hiyo ya Rais na kama haitaviathiri vyama kikiwemo chama anachokiongoza cha TLP.

''Kwa maoni yangu binafsi hii imetokana na tabia yetu sisi wapinzani kugomea kila kitu hata mambo ambayo yana maslahi kwa taifa, kwa mfano ukiangalia wakati Rais Dkt. John Magufuli anazindua bunge la bajeti wapinzani walimgomea na kutoka nje, hapa walianza kumhukumu kabla hajaanza kazi''- Amesema Mrema.

Mrema ameongeza kuwa hata bunge la bajeti linaloendelea wabunge wa upinzani wametoka vikao karibu vyote wakati bajeti inayojadiliwa siyo ya Naibu Spika ni bajeti ya serikali na kwamba wangetumia kanuni za bunge kuweza kumuondoa kama hawamtaki kuliko kuacha kuwakilisha wananchi wao.

Aidha Mrema ameenda mbali na kusema kuwa nchi hii haiwezekani kila siku ikawa ni maandamano kwani wananchi wanatakiwa wafanye kazi na kama wapinzani walikuwa na nia ya dhati wangebakia bungeni wajadili kwanza bajeti.

Kuhusu chama chake pia kutofanya siasa Mrema amesema yeye hana maandamano ya kila mara hivyo anaamini atakuwa na mikutano halali muda ukifika lakini kwa sasa wananchi wafanye kazi kwanza.