Vanessa Mdee aendelea kusota mahabusu


Kamishna wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Siro amesema jeshi hilo bado linamshikilia Msanii maarufu wa mziki wa kizazi kipya, Vanessa Mdee ambaye alikamatwa siku ya Jumatano kwa tuhuma za kutumia na kusambaza dawa za kulevya.
Kamishna Sirro ameyasema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo alieleza kuna watu wengi wanaoshikiliwa kwa tuhuma za kujihusisha na dawa hizo akiwepo msanii Rumishaeli ambaye ni maarufu kwa jina la Rummy.
“Juzi tulimkamata Vanesa Mdee na taarifa zinaonyesha ni mtumiaji na msambazaji lakini upelelezi unaendelea na ukikamiliki tutamfikisha mahakamani au tutamuachia. Na sio hao tu wapo wengine ambao tuna majina baadhi tumewakamata inasemekana huwa wanasafirisha dawa hizo kwenda Afrika Kusini,” amesema Siro.
Vanessa Mdee alikuwa miongoni mwa watuhumiwa waliotajwa katika orodha ya awamu pili iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda lakini hakuweza kuripoti kwa wakati kutokana na kuwa nje ya nchi kikazi.