Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, amesema akiwa magereza amewakuta watoto wadogo, mmoja wa miaka 14 ambaye amefungwa mwaka mmoja kwa kukutwa na bangi na tayari taarifa zake amepeleka kwa Msajili wa Mahakama Kanda ya Arusha.
Lema aliyasema hayo jana mbele ya maelfu ya wakazi wa Jiji la Arusha waliojitokeza katika mkutano wake wa kwanza tangu atoke gerezani, kwa dhamana.
Machi 3, mwaka huu, Lema aliachiwa kwa dhamana baada ya kukaa gerezani miezi minne tangu alipokamatwa akiwa bungeni mjini Dodoma, Novemba mwaka jana.
Alisema ameshuhudia pia vijana 65 wa Jiji la Arusha ambao wamekaa miaka minne gerezani kwa tuhuma za ugaidi na kwamba, hadi sasa kesi yao haijaanza kusikilizwa na wamekuwa wakiteswa hadi mmoja kuvunjwa mguu.
“Ndugu zangu kukaa magereza kumenipa ujasiri mkubwa na kumesaidia kujua shida za watu, kwani kuna watu wamefungwa maisha kwa kukutwa na mirungi wakati nchi jirani Serikali inatoa fedha kupanua mashamba ya mirungi,” alisema lema.
Mbunge huyo alisimulia mwanzo mwisho mambo aliyojionea gerezani kwa muda wa miezi minne aliyokaa huko.