Kikwete Aja na Foundation Yake,Imesheheni Vigogo wa Afrika na Dunia...!


RAIS Mstaafu, Jakaya Kikwete, kesho anatarajiwa kuzindua Taasisi ya Maendeleo ya Jakaya Mrisho Kikwete Foundation (JMKF), kabla hajazungumza na wanahabari kwa mara ya kwanza tangu amalize muda wake wa uongozi Oktoba 2015.

Taarifa iliyotolewa na taasisi hiyo, ilisema Kikwete baada ya kuzindua taasisi hiyo pamoja na bodi ya udhamini, atazungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam ikiwa ni mara yake ya kwanza ndani ya miezi 16 tangu amalize kipindi cha miaka 10 ya uongozi wake.

“Taasisi hii iliyosajiliwa nchini, itakuwa chini ya uongozi wa bodi ya wadhamini wa kimataifa wa ndani na nje wakiwamo kutoka Marekani, Tanzania na Guinea Bissau,” ilisema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo iliwataja wajumbe wa bodi ya wadhamini wa taasisi hiyo wa ndani ya nchi ni Ombeni Sefue, aliwahi kuwa Katibu Kiongozi wa Utawala wa Kikwete na Rais John Magufuli, Prof. Rwekaza Mukandala ambaye ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Willaim Mahalu na Balozi Mwanaidi Maajar.

Wengine walitajwa ni Genevieve Sangundi, Abubakar Bakhresa, Mkurugenzi Mtendaji wa kundi la makampuni ya Carlyle Afrika Kusini na mjumbe wa bodi ya wakurugenzi ya Benki Kuu ya Nigeria.

Wamo pia Balozi wa zamani wa Marekeni nchini, Charles Stith, Dato Sri Idris Jala (Waziri asiyekuwa na wizara maalum Ofisi ya Waziri Mkuuwa Malaysia) na Dk. Carlos Lopez wa Guinea Bissau ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa taasisi ya mafunzo ya Umoja wa Mataifa (UNITAR).