Imefichukaaa..Huu Hapa Mkakati Mzito Unaosukwa Zanzibara wa Kumfuta Kabisa Maalim Seif,Yadaia Unasukwa Kitaalamu na Wajuzi Waliobobea Ikiwemo Bunge...!!!


IKIWA Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad bado ana ndoto za kugombea tena urais katika uchaguzi mkuu ujao basi anapaswa kazi ya ziada.

Hali hiyo imejidhihirisha baada ya mmoja wa mawaziri katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (smz) kuelezea mpango wa kupitisha sheria itakayomuondoa jumla Waziri Kiongozi na makamu wa kwanza wa rais huyo wa zamani kabla ya uchaguzi ujao utakaofanyika mwaka 2020.

Akielezea jambo hilo wakati akizungumza  katika mahojiano maalumu juzi, Waziri asiyekuwa na Wizara Maalumu wa Zanzibar, Said Soud Said, alisema, Maalim Seif atalazimika kuwapisha vijana katika uchaguzi mkuu ujao na asahau kabisa uwezekano wa yeye kugombea tena kwa sababu wakati huo (mwaka 2020), tayari kutakuwa na sheria inayozuia mtu yeyote aliyetimiza miaka 70 kugombea urais visiwani humo.

“Maalim Seif ameshapoteza uwezo wa kuwa rais kwa sababu sisi tunataka kupeleka hoja katika Baraza la Wawakilishi kuhakikisha mtu mwenye umri wa miaka 70 hagombei urais,” alisema Soud ambaye ni Mjumbe wa Baraza la Wawawkilishi wa kuteuliwa na pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima (AFP).

Akifafanua zaidi suala hilo, Said alisema: “Hoja ya msingi ni kuwafanya vijana wanaosoma katika nchi hii waweze kushika nafasi na kuiongoza Tanzania… na Zanzibar na tuna vijana wazuri tu. Hebu tuangalie utendaji kazi wa vijana.

“Mimi naamini Maalim Seif ameshapoteza uwezo wa kuongoza Zanzibar na sasa kazi iliyobakia (kwake) ni kuwa mwanasiasa ambaye anaweza kutoa ushauri…lakini kwa hoja ya kuwa Rais wa Zanzibar hana nafasi nayo tena.”

Akizungumzia jambo hilo, Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Zanzibar), Nassoro Mazrui, alisema hatua hiyo itakuwa ni kichekesho cha mwaka kwa sababu katiba inaeleza wazi juu ya sifa za watu wanaostahili kugombea urais na kingine, ni ukweli kwamba siyo Maalim Seif wala mtu yeyote mwenye uhakika wa kuiona 2020 na kisha kupitishwa na chama chake kugombea urais.

Kabla ya kuwania tena nafasi hiyo kwenye uchaguzi wa mwaka 2015 ambao ulifutwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kwa kile kilichoelezwa na mwenyekiti wa tume hiyo, Jecha Salim Jecha, kwamba kulikuwa na kasoro nyingi, Maalim aliwahi pia kugombea urais wa visiwa hivyo katika miaka ya 1995, 2000, 2005 na 2010.

Katika chaguzi zote hizo, Maalim Seif alikuwa akichuana vikali na chama tawala (CCM) na mwishowe kuingia madarakani kama makamu wa kwanza wa Rais baada ya uchaguzi wa 2010, hiyo ikiwa ni baada ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Hata hivyo, Maalim Seif na chama chake (CUF) hawakushiriki uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20, 2016, wakidai ni batili na badala yake kusisitiza kuwa ZEC iendelee kujumuisha matokeo ya uchaguzi wa awali uliofanyika Oktoba 25, 2015 ambao wao walishinda kwa zaidi ya asilimia 50.

AMSIFU DK. SHEIN KUIPAISHA ZANZIBAR
Katika hatua nyingine, Said alisifu uongozi thabiti wa Rais Dk. Shein kutokana na mafanikio makubwa yanayoonekana karibu katika kila nyanja, baadhi zikiwa ni za afya, elimu, viwanda na pia kuendelea kudumu kwa amani na utulivu visiwani humo.

“Mwaka mmoja, tayari Dk. Shein ameshaonesha mwelekeo na kutekeleza mambo mengi mazuri ambayo aliyaahidi wakati wa kampeni,” alisema Said na kuongeza:

“Ameweza kufanikiwa kuwalinda Wazanzibari na kuwafanya kuwa kitu kimoja, ameweza kuondosha tofauti zao katika shughuli mbalimbali za kiutendaji na kimaisha kama harusi, mazishi na hata kusafiri katika chombo kimoja bila ya kubaguana.

Kwa upande wa maendeleo ameonyesha mwelekeo mpya kwa kuwapatia Wazanzibari hospitali za kisasa. Ameweza kuendeleza utaratibu wa kuwapatia wazee pesa za kujikimu kila mwezi.

“Dk. Shein ameweza kufungua milango ya ajira kwa vijana wengi bila ya kujali vyama, rangi wala dini zao bali (huwaajiri) kutokana na elimu ya mtu mwenyewe.

Ahadi iliyotolewa na Rais wa kwanza wa Zanzibar Mzee Karume ikiwamo elimu bure, afya bure na upatikanaji wa maji safi na salama, Dk. Shein anaendelea kuyaendeleza hayo licha ya kuwapo kwa changamoto ndogondogo.”

Aidha, Said alisema kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja, Dk. Shein amefanikiwa kuiamrisha usafiri wa Unguja na Pemba na sasa wananchi wa visiwa hivyo wanaweza kusafiri na kurudi walikotoka kwa siku moja, wakitumia boti na ndege.

“Dk. Shein katika kipindi cha mwaka mmoja ameboresha mishahara ya kima cha chini na kuiongeza kwa asilimia 100, ameifanya Zanzibar kuwa ya viwanda kwani kuna kiwanda cha sukari na maziwa… hayo yote ni maendeleo ya mwaka mmoja tu wa Dk. Shein.

“Ninachowaomba Wazanzibar ni kutoa ushirikiano kwa Serikali licha ya (tofauti) ya itikadi ya vyama... upinzani siyo uadui bali ni changamoto zinazomfanya aliyekuwapo juu kuelekezwa namna ya kuleta maendeleo,” alisema Said.

TUHUMA AFP KUTUMIWA NA CCM
Alipoulizwa kuhusu madai kwamba chama chake cha AFP hutumiwa kama kibaraka wa CCM na ndiyo maana hivi sasa kipo kimya, Said alipinga madai hayo na kusisitiza kuwa anachokifanya sasa ni kushiriki katika kutekeleza ilani ya CCM ambayo ndiyo inayoongoza serikali.

“AFP haipo kimya. Mimi hivi sasa natekeleza ilani ya CCM na nitaendelea kuitekeleza ilani ya CCM mpaka tume ya uchaguzi itakapotangaza uchaguzi mwingine mwaka 2020,” alisema Soud.

Akifafanua zaidi, Said alisema kuwa hivi sasa, yeye na chama chake hawasikiki kwa sababu wanasubiri uchaguzi ndipo wafanye hivyo.

“Ilani zangu za AFP nitazitoa katika koti… lakini kwa sasa zimo ndani ya koti na hazina nafasi mpaka pale tume itakapotangaza uchaguzi 2020.

Hapo ndipo nitakuwa huru kutumia sera na ilani ya AFP. Lakini kwa sasa nitaendelea kutumikia ilani ya CCM ambayo ndiyo inayoongoza serikali,” alisema Soud ambaye katika uchaguzi mkuu wa marudio alijitosa kuwania urais na kwa mujibu wa ZEC, alipata kura 1,303 kati ya kura 328,327, sawa na asilimia 0.4. Dk. Shein wa CCM alitangazwa mshindi kwa kupata asilimia 91.4.

Said alizaliwa Pemba mwaka 1949 na kuanza kujihusisha na siasa akiwa na umri wa miaka 18. Elimu yake ni ya kidato cha nne.