HUKU kukiwa na taarifa kwamba ndoa yake na msanii wa Bongo Fleva, Hamis Ramadhan Baba ‘H-Baba’ imeparaganyika, mrembo wa Bongo Movies, Flora Mvungi amedaiwa kunasa kwenye penzi la mmoja wa mawaziri wa serikali ya awamu ya tano.
Chanzo kilicho karibu na msanii huyo kimepenyeza habari kuwa, mrembo huyo kwa sasa yupo chini ya himaya ya waziri huyo (jina kapuni kwa kuwa hatujampata) ambapo safari ya uhusiano wao ilianzia mjini Dodoma.
“Nakumbuka ilikuwa ni mwaka jana, Flora alienda Dodoma na wasanii wenzake sasa alipofika mjengoni, waziri aliuona
mzigo hivyo akaomba nafasi na Flora bila hiyana akakubali.
“Mwanzoni kidogo alichomoachomoa lakini waziri alimuahidi maisha mazuri, na kwa kuwa tayari walikuwa kwenye gogoro na mtu wake(H-Baba), ilikuwa ni kama kumsukuma mlevi tu. Mtoto wa kike akaingia mzimamzima, yani sasa hivi Flora, kafa kaoza kwa mheshimiwa,” kilisema chanzo hicho makini.
Jitihada za kumpata waziri huyo ziligonga mwamba kufuatia simu yake ya mkononi kutokuwa hewani. Atakapopatikana, tutaripoti kwa upande wake ili kujua anazungumziaje madai hayo.
Kwa upande wake Flora, alipotafutwa na mwanahabari wetu alikiri kukutana na waziri huyo Dodoma lakini akaomba asizungumzie suala hilo kwani litamweka kwenye nafasi mbaya katika jamii.
“Naomba sana mliache hilo suala, najua aliyevujisha lakini nawaombeni sana mliache kabisa. Litanichafua tafadhalini sana,” alisema Flora.