Jeshi La Polisi Lamshikilia Mwanamke Mmoja Kwa Tuhuma Za Kutupa Mtoto Chooni

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, linamshikilia, Mwananke mmoja alietambulika kwa jina la Rosemary Khiwili (23) mkazi wa Kimara  kwa kosa la kutupa mtoto katika shimo la choo.

Rosemary ambaye ni mfanyakazi wa Hoteli ya Landmark jijini Dar es Salaam anadaiwa kumtupa mtoto mchanga katika choo cha shimo cha nyumba anayoishi na mtoto huyo amegundulika na mama mwenye nyumba, Upendo Mboma baada ya kuingia kwa ajili ya kumwaga maji machafu na ndipo aliposikia mtoto analia kutokea kwenye choo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishina wa Jeshi la Polisi (CP), Simon Sirro amesema kuwa tukio hilo lilitokea Juni 8 mwaka huu huko maeneo ya Kimara Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Kamishina, Sirro amesema mtoto huyo aliokolewa na akiwa hai na kikosi cha Zimamoto na uokoaji  cha jiji kwa kushirikiana na askari polisi , na mtoto huyo amehifadhiwa katika hospitali ya Mwananyamala kwa uangalizi maalum huku upelelezi ukiendelea na ukikamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi.

Wakati huo huo jeshi la polisi limeokota silaha mbili zilizotengenezwa kienyeji  pamoja risasi sita  zikiwa kwenye begi katika shamba la matuta ya viazi baada kutelekezwa na watu wasiojulikana na jitihada zinaendelea kuwabaini watu hao.

Kamanda, Sirro amesema katika operesheni ambayo wanaifanya kwa wiki hii wameweza kuwakamata watu 711  kwa makosa ya unyang’anyi wa kutumia nguvu, kukutwa bhangi na Gongo , mitambo ya kutengeneza gongo, kucheza kamari pamoja na biashara ya kuuza mwili.

Amesema  Kawe pamoja na Mabibo zinaongoza kwa utengenezaji na uuzaji wa pombe haramu ya Gongo.