Hii ni Picha iliyosambazwa katika mitandao ya kijamii ikidai kuwa Gwajima kafariki dunia na yuko Mochwari.Taarifa hizi zilimpa hofu Gwajima na kumfanya Aagize Bastola yake kwa ajili ya kujihami. |
Utata umeibuka kuhusu bastola waliyodaiwa kukamatwa nayo wafuasi wa Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima baada ya kiongozi huyo kusema anaimiliki kihalali kinyume na maelezo ya polisi.
Gwajima aliyetolewa kwenye chumba cha uangalizi maalumu cha Hospitali ya TMJ jana, amelitaka Jeshi la Polisi kurudisha bastola hiyo, akisema ni mali yake na aliiagiza ipelekwe hospitalini kwa sababu ya kujilinda.
Akizungumza na waandishi wa habari hospitalini hapo alipolazwa baada ya kuishiwa nguvu na kupoteza fahamu akiwa katika mahojiano na polisi, Gwajima alisema anashangaa kukamatwa kwa wachungaji wake waliokuwapo kwa ajili ya kumlinda.
Hata hivyo, katika kwa upande mwingine, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema bunduki hiyo haina umiliki halali wa Gwajima wala wa wachungaji 15 waliokamatwa lakini baadaye jioni baada ya maelezo ya Gwajima, alitoa taarifa akisema bastola hiyo ni mali halali ya askofu huyo. Pia alisema kuhusu risasi 17 za bunduki aina ya Shortgun, Gwajima anamiliki bunduki ya aina hiyo lakini akasema uchunguzi kuhusu watu hao 15 unaendelea.
Kauli ya Gwajima
Akizungumza kwa shida akiwa amejishika tumbo, Gwajima alisemaalipopata taarifa za uvumi kwenye mitandao ya kijamii kuwa amefariki dunia, aliagiza wachungaji waende hospitalini kwa ajili ya kumlinda, lakini wakaishia mikononi mwa polisi wakidaiwa kutaka kumtorosha.Kauli ya Gwajima
Alisema alihofia kuwapo kwa watu wabaya ambao wangeweza kumdhuru halafu wakasingizia kitendo hicho kufanywa na polisi kwa kuwa alipata tatizo akiwa mikononi mwao.
“Usiku wasiwasi ulizidi, huku kila mmoja akiwa hafahamu kwa nini ujumbe wa namna ile unasambazwa kwenye mitandao, msambazaji ni nani, ana nia gani, nikaamua kuwaagiza waniletee silaha yangu iliyokuwa kwenye begi ili likitokea lolote niweze kujilinda,” alisema Gwajima.
Alisema alishangaa kukamatwa wachungaji wake na kuchukua silaha iliyokuwa ndani ya begi na hadi jana hakuwa ameulizwa chochote kuhusu umiliki wa silaha hiyo.
“Kabla sijazungumza na waandishi kueleza ukweli wa kinachodaiwa kuwa nilitaka kutoroshwa na wachungaji wangu, nilitaka kuzungumza na ZCO (Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu), lakini hajaja, kadi ya ile silaha ninayo,” alisema Gwajima.
Alisema madai kuwa alitaka kutoroka ilihali polisi alikwenda mwenyewe akitokea Arusha baada ya kusoma katika vyombo vya habari kuwa anatafutwa.
Alifafanua kuwa hata alipofika polisi kwa ajili ya mahojiano hakuwa na shaka hata kidogo, lakini alishangaa kuona anaishiwa nguvu kila baada ya muda na alipoona kichwa kinamuuma, akawaomba wampeleke hospitali ili mambo mengine yafuate baadaye, kitu ambacho hakikufanyika kwa wakati.
Wasiwasi kwa polisi
Alisema alijaribu kuomba apelekwe hospitali mara kadhaa, lakini hakuna aliyekubaliana naye hadi alipopoteza fahamu na kupelekwa hospitali ya Polisi Kurasini.
“Hivi hata kama ni chombo cha usalama, nimepata matatizo nipo mikononi mwao, halafu nikubali kutibiwa katika hospitali yao, sikulitaka hilo na hata waliposema nikatibiwe Muhimbili pia sikutaka, ndiyo maana nilikuja hapa, sisemi moja kwa moja kama Polisi wanahusika lakini kuna vitu vinanitia shaka,” alisema Gwajima.
Alieleza kuwa anatilia shaka Jeshi la Polisi kutokana na kuwapo vitu vingi vinavyoashiria wana kitu kingine wanatafuta, kwani jana tulikuwa na hofu ya kuvamiwa, waliokuja kutuvamia ni wao, sikugombana na Pengo, nilikuwa namkemea kama kiongozi mwenzangu wa kiroho wao, wameligeuza ni kesi.
“Sijawahi kulitilia shaka Jeshi la Polisi lakini katika hili napata wasiwasi mwingi, sina ugomvi na Kardinali Pengo, nampenda, hajanilaumu, wala kunishtaki, nilikuwa namkemea katika masuala yetu ya mabaraza ya dini na siyo vinginevyo,” alisema Gwajima.
Gwajima pia alionyesha wasiwasi wake kwa kile kilichokuwa kinang’ang’aniwa na polisi kwenda kupekua nyumbani kwake kuwa hakikuwa kitu kizuri.
Kova alipinga
Wakati Gwajima akisema hayo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema bastola waliyokutwa nayo wafuasi wa Gwajima haimilikiwi kihalali.
“Tumegundua kuwa katika wale watu waliokuwa pale akiwamo Gwajima mwenyewe, (bastola) haikuwa katika umiliki wao halali, kwa hiyo hapa kuna kesi ya kupatikana na silaha bila kibali.”
Akizungumzia tuhuma kwamba polisi walimpekua mke wa Gwajima, Kova alisema hakuna polisi waliofika nyumbani kwake kufanya upekuzi wowote na kama wakitaka kufanya hivyo watafuata taratibu maalumu za upekuzi.
Akijibu swali kuhusu mahali Gwajima alipotakiwa kutoroshewa, Kova alisema uchunguzi huo bado unaendelea na utakapomalizika wahusika watafikishwa mahakamani.
Pia alipoulizwa kama Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amemsamehe Gwajima, kwani polisi imng’ang’anie, Kova alisema;“amesema anamsamehe lakini haingilii mambo ya sheria.”
Kuhusu sababu za Gwajima kuzimia wakati akihojiwa, Kova alisema anayepaswa kuulizwa kwa nini alianguka wakati akihojiwa na polisi ni Gwajima mwenyewe.
“Siri za mahojiano huwa hazitolewi kabla ya ushahidi mahakamani, sababu ya kupata shock (mshtuko) atajua mwenyewe, kwa kuwa ukifanyiwa jambo ukafurahi au ukachukia wewe ndiyo unajua ilikuwaje, chochote kitakachotokea ukicheka, ukinuna, ukizimia, wewe ndiyo tukuulize ilikuwaje mpaka ukazimia kwa sababu hisia unazipata wewe,”alisema Kova.
Makonda amtembelea
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda ambaye alikuwa amemwandikia Gwajima barua akimwita ofisi kwake, jana mchana alimtembelea hospitalini hapo kwa ajili ya kumjulia hali kiongozi huyo lakini akasisitiza kuwa nia yake bado ipo palepale.
“Nilimtaka leo aripoti ofisini kwangu lakini kwa bahati mbaya anaugua na amelazwa. Nitakwenda kumuona ili nijue hali yake ikoje,” alisema Makonda kabla ya kufunga safari kwenda hospitali alikolazwa.
Alisema pia atataka kiongozi huyo wa kiroho amweleze anavyoelewa maana ya uhuru wa kuabudu unaoelezwa katika Katiba, usajili wa taasisi yake na katiba ya taasisi hiyo.
“Mimi ni mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kinondoni. Niliagiza polisi wamkamate na baadaye wakimaliza kumhoji aje kwangu pia atahojiwa na jopo la watu 20,” alisema Makonda.
“Mimi ni mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kinondoni. Niliagiza polisi wamkamate na baadaye wakimaliza kumhoji aje kwangu pia atahojiwa na jopo la watu 20,” alisema Makonda.